Waiacha Yanga kwenye mataa
MTEGO
waliouweka Simba katika kambi yao ya wiki moja kisiwani Unguja,
unaonekana kuzaa matunda kiasi ambacho hata kama Yanga ilituma
mashushushu wa kuipeleleza kimya kimya wataondoka wakiwa na taarifa
chache mkononi tofauti na walivyotarajia.
Simba
inayorejea jijini Dar es Salaam leo Jumatatu kwa boti, benchi lake la
ufundi limefanya mambo mawili ambayo yanaiumiza kichwa Yanga kutafuta
namna ya kupambana nayo kabla ya timu hizo kukutana kwenye mechi ya Ngao
ya Jamii keshokutwa Jumatano.
Kwanza imeipa Yanga
kazi ya kufahamu majina ya wachezaji watatu kati ya 11 ambao watakuwamo
kwenye kikosi cha kwanza cha Simba watakachokutana nacho kwenye mechi
hiyo.
Hadi sasa Mwanaspoti inafahamu wachezaji wanane
ambao bila shaka watakuwemo kwenye kikosi cha kwanza ambacho kitacheza
na Yanga, kutokana na mechi za kirafiki na mazoezi ambayo Simba imekuwa
ikiyafanya kisiwani hapa kujiandaa na mchezo huo, lakini majina matatu
yamebakia kuwa siri nzito ya benchi la ufundi la Simba chini ya
Mkameruni, Joseph Omog.
Wachezaji ambao wataipa ugumu
Yanga kufahamu watacheza kwenye nafasi zipi keshokutwa ni Haruna
Niyonzima, Erasto Nyoni na Shiza Kichuya ambao wamekuwa wakichezeshwa
katika nafasi tofauti tofauti mazoezini na kwenye mechi za kirafiki.
HAWA PIGA UA WAMO
Wachezaji
ambao ni uhakika watacheza Jumatano labda mambo yabadilike ndani ya leo
Jumatatu na kesho Jumanneni Aishi Manula, Method Mwanjali, Salim
Mbonde, Erasto Nyoni, Shiza Kichuya, Muzamiru Yassin, Haruna Niyonzima
na Emmanuel Okwi.
Nyota hao ndio ambao wameonekana
kupewa muda mwingi wa kucheza katika mechi za kirafiki ambazo Simba
ilicheza dhidi ya Mlandege na Gulioni FC lakini pia hata kwenye mazoezi
ya timu hiyo, wachezaji hao wanane ndio wamekuwa wakifuatiliwa kwa
umakini wa hali ya juu na benchi la ufundi.
Nafasi moja
ya beki wa pembeni, moja ya ushambuliaji na ya kiungo mkabaji ndizo
ambazo hadi sasa haijajulikana ni nani hasa watakaopewa nafasi ya
kuzicheza katika mchezo huo.
Iwapo Simba wataamua
kuanza na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ upande wa beki wa kushoto, ni
wazi kuwa Erasto Nyoni atacheza beki wa kulia, lakini kama beki huyo
Tshabalala hatacheza, Nyoni atacheza kushoto huku nafasi ya beki wa
kulia ikichezwa na Ally Shomary.
Kwa kiungo mkabaji,
Simba wanaweza kuanza na James Kotei au Jonas Mkude kulingana na mipango
ya benchi la ufundi lakini pia hata Erasto Nyoni naye anaweza kucheza
nafasi hiyo.
Kwenye ushambuliaji, Simba wana uhakika wa
kumtumia Emmanuel Okwi kwa namba yoyote kati ya 9, 10 au 11 na hivyo
kuliachia jukumu benchi la ufundi kuchagua nani aanzishwe kati ya Juma
Luizio au Laudit Mavugo kulingana na mfumo.
Kingine
ambacho Simba wamekifanya ni kuwachezesha baadhi ya wachezaji katika
nafasi tofauti, jambo linalowapa ugumu Yanga kufahamu hasa halisi ambazo
baadhi ya wachezaji watacheza siku hiyo.
Hata hivyo,
kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema: “Timu ina kikosi
kipana ambacho kitakuwa na faida kwetu kwenye ligi na mashindano ya
kimataifa ambayo tutashiriki mwakani. Tumekuwa tukibadilisha na
kuwapanga wachezaji kwenye nafasi tofauti ili kuona nani anafiti wapi na
akicheza na nani.
“Mechi ya Yanga, tunaweza kumpanga
mchezaji yeyote yule na tukaweza kupata matokeo kwa sababu tuna kundi
kubwa la wachezaji wenye uwezo mkubwa,” alisema Mayanja.
No comments